Yohane Krisostomo

Yohane Krisostomo ( karne XI.
Yohane Krisostomo na Gregori wa Nazianzo katika picha ya Kirusi ya karne XVIII.

Yohane Krisostomo, kwa Kigiriki χρυσόστομος, khrysóstomos, yaani «Mdomo wa dhahabu» alivyoitwa kutokana na ubora wa mahubiri yake, ( Antiokia wa Siria, leo Antakya,nchini Uturuki, 347 hivi - Comana Pontica, Uturuki, 14 Septemba 407) alikuwa Patriarki wa Konstantinopoli.

Ari yake ilisababisha apendwe na vilevile achukiwe sana. Hatimaye alifukuzwa na Kaisari na kufa uhamishoni.

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1568 Papa Pius V alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 14 Septemba.

Maisha

Asili na ujana

Yohane alizaliwa Antiokia wa Siria katika familia tajiri ya Kikristo mwaka 347 hivi. Wakati huo mji huo ulikuwa unamfuata Konstantinopoli na Aleksandria tu kwa umuhimu upande wa mashariki wa Dola la Roma.

Katika karne IV huko zilitokea vurugu nyingi kwa msingi wa dini. Mjini kulikuwa na ma askofu wawili walioshindana: Melesyo na Paulino. Yohane aliishi ujana wake katika mazingira hayo, akikosa utulivu, akipenda vyakula na maigizo.

Baba yake, Sekundo, aliyekuwa askari kiongozi, alifariki mapema na kumuacha mtoto mdogo pamoja na dada yake kwa mama yao, Anthusa, mwenye umri wa miaka 22 tu ambaye alimlea vizuri sana upande wa utu na wa imani vilevile.

Baada ya masomo yote, alifundishwa tena na Libanio, mhubiri maarufu kuliko wote wa wakati ule ingawa Mpagani, ambaye alisema juu yake, «Angekuwa kati ya wanafunzi wangu bora, kama Kanisa lisingeniibia». Kumbe Yohane akaja kumzidi, ila upande wa kuhubiri Neno la Mungu.

Alipofikia miaka 18 anni alikutana na askofu Melesyo akamuomba ubatizo (alioupata mwaka 368) akaanza kufuata kozi za Diodoro wa Tarso, maarufu kwa ufafanuzi wa maneno yenyewe ya Biblia usiofuata sana maana ya kiroho.

Kupewa daraja

Alipomaliza masomo hayo ( 367- 372) na kupewa daraja ndogo akajifungia upwekeni miaka minne akasoma teolojia, hasa Injili na Nyaraka za Mtume Paulo. Katika pango alimoishi miaka miwili tena, afya yake ikawa mbovu ikamrudisha Antiokia kwenye wito wake halisi: uchungaji. Uzoefu wa kutafakari Neno la Mungu upwekeni ulikuwa umestawisha ndani yake msukumo mkubwa wa kushirikisha wengine kwa kuhubiri Injili.

Alitunga kitabu juu ya upadri kilichoathiriwa sana na Gregori wa Nazianzo. Humo alieleza kuwa umonaki si njia pekee ya kulenga ukamilifu; bali kutoa huduma za kipadri kwa faida ya waamini kati ya vishawishi vingi vya ulimwengu ndiyo njia bora ya kumtumikia Mungu. Aliandika kwamba angetakiwa kuchagua kati ya matatizo ya kuongoza Kanisa na utulivu wa maisha ya kimonaki angechagua mara elfu huduma ya kichungaji.

Miezi ya baridi kati ya miaka 380381 alipewa na Melesyo daraja ya u shemasi mwaka 386 na miaka michache baadaye akawa kasisi na msaidizi mkuu wa askofu Flaviano, akihubiri katika kanisa muhimu zaidi la Antiokia.

Wakati huo alisema, “Anatosha mtu mmoja mwenye ari kwa kubadilisha mwenendo wa umati”. Maneno hayo yakawa kaulimbiu yake kama mchungaji na kiongozi wa kiroho wa watu wake akiwatia moyo kufuata maadili.

Sifa yake kama mhubiri iliongezeka, hasa Antiokia ilipokabili ghadhabu ya Kaisari kwa uasi wa mwaka 387, hata wasikilizaji wakaanza kujiandikia kumbukumbu za maneno yake.

Pamoja na hayo mwenyewe aliendelea kutunga vitabu mbalimbali.

Mwaka 397 Patriarki Nektario alipofariki, kulikuwa na ushindani mkubwa kwa kushika nafasi yake, mpaka Kaisari Arcadio, kinyume cha matarajio ya wote, alipomchagua Yohane, ambaye hakuwa na hamu hiyo.

Alihamia huko kwa kutumiwa tu nguvu na udanganyifu, bila kujua namna ya kuhusiana na vigogo.

Askofu

Huko Konstantinopoli aliongoza Kanisa kwa bidii nyingi ili kulirekebisha, akishambulia ufisadi na anasa ya viongozi, akijipatia hivyo maadui wengi kwenye ikulu. Hivyo maisha yake hayakuwa na amani, tofauti na hamu ya moyo wake mpole.

Mwenyewe aliishi kwa usahili, unyenyekevu na uchangamfu kama kielelezo kwa wote, akitumikia watu na kutumia mali zake kwa ajili ya ma fukara na wagonjwa.

Aliendelea kushika maisha magumu na kudai wasaidizi wake pia wafanye vilevile. Kwa usimamizi wake mzuri alianzisha na kuendesha miundo mbalimbali ya misaada, hata akaitwa “Mtoasadaka”.

Isitoshe, katika mahubiri yake alipendekeza Kanisa la Konstantinopoli lifuate kielelezo cha lile la kwanza la Yerusalemu na hivyo lichangie ujenzi wa jamii mpya ambapo wote waishi kama ndugu: hakuna wa kuachwa nyuma, kwa kuwa kila mmoja ni muhimu, si jamii tu. Hivyo alichangia sana mafundisho ya Kanisa kuhusu masuala ya jamii.

Kama mchungaji halisi, aliwatendea wote kwa wema, akiheshimu wanawake kwa namna ya pekee na kuwajibika kwa ustawi wa ndoa na familia.

Alihimiza waamini washiriki katika liturujia, aliyoipamba kwa ubunifu izidi kupendeza.

Alipambana kwa nguvu na uzushi na kuleta nidhamu katika majimbo yaliyo chini yake, akiwafukuza mapadri wengi wasiofaa, na hata askofu wa Efeso na wengine watano waliopata madaraka kwa dhambi ya usimoni. Kwa hilo alilaumiwa kuwa alitumia mamlaka nje ya mipaka yake.

Pia alilazimisha wamonaki wazururaji warudi katika monasteri zao, ila alipokea wengine kutoka Misri waliokuwa wametengwa na Kanisa kwa uamuzi wa Patriarki Teofilo wa Aleksandria, ambaye alichukia hilo pia.

Mwanzoni alitegemezwa na ikulu, lakini baada ya kumlaumu malkia Eudoksia kwa kujipatia mali ya mjane na kuishi kwa anasa, uhusiano uliharibika, akazidi kusingiziwa na kutukanwa.

Mwaka 402 maadui wake wengi, wakiwemo maaskofu, waliomba msaada wa patriarki Teofilo wa Aleksandria, ambaye Kanisa lake lilikuwa na ushindani na yale ya Konstantinopoli na Antiokia. Teofilo mwenyewe alikuwa amelazimika kujitetea katika sinodi iliyoongozwa na Yohane kuhusu mashtaka ya wamonaki dhidi yake.

Basi, mwaka 203 katika sinodi ya Mwaloni, karibu na Kalsedonia, Teofilo alifika pamoja na maaskofu saba wa Misri na wengine 29 waliokuwa wote upande wake, akamfanya Yohane afukuzwe na Kaisari, ila kesho yake malkia alimrudisha baada ya umati kudai hivyo kwa nguvu.

Miezi miwili baadaye uhusiano wa Yohane na Eudoksia ulichafuka tena, askofu alipolaumu ujenzi wa sanamu ya malkia karibu na kanisa, hata alisema maadhimisho kwa ajili yake yalikuwa ya kipagani akamfananisha na Herodia mwenye hamu na kichwa cha Yohane Mbatizaji.

Hivyo masingizio na njama viliendelea hata aliomba msaada wa Papa Inosenti I na maaskofu wengine muhimu wa magharibi, lakini huo haukuweza kuwahi: mtaguso, uliotakiwa na Kanisa la Roma ili kupatanisha pande mbili za Dola na makanisa yake yote, haukuweza kufanyika.

Uhamishoni

Basi, tarehe 9 Juni 404 Yohane alifukuzwa jimboni moja kwa moja. Kwa miaka mitatu aliishi Kukuso, kwenye milima ya Armenia, akitenda kazi kubwa hata kwa kuandika barua nyingi ili kuwatia moyo wafuasi wake waliodhulumiwa vilevile.

Halafu mwaka 407, kutokana na wingi wa watu waliomtembelea, alihamishwa tena aende mahali pagumu zaidi, huko Pitiunte, mashariki kabisa kwa Bahari Nyeusi, lakini tarehe 14 Septemba 407 alifariki huko Comana Pontica akiwa njiani.

Maneno yake ya mwisho yalikuwa: "Utukufu kwa Mungu kwa yote. (Doxa to Theo pantôn eneke)."

Mwaka 438 Kaisari mwingine, Theodosi II alirudisha masalia yake Konstantinopoli ambako yalipokewa na umati kwa shangwe.

Maandishi yake ni mengi sana, kuliko ya mababu wengine wote wa Kigiriki. Sehemu kubwa ni mahubiri (zaidi ya 700) aliyoyatoa kwa kawaida wakati wa liturujia, vitabu vya ufafanuzi wa Biblia, vya teoloja n.k. mbali ya barua 241 zilizotufikia.

Other Languages
asturianu: Xuan Crisóstomu
azərbaycanca: İohann Xrisostom
беларуская: Іаан Златавуст
български: Йоан Златоуст
čeština: Jan Zlatoústý
Cymraeg: Ioan Aurenau
français: Jean Chrysostome
hrvatski: Ivan Zlatousti
Bahasa Indonesia: Yohanes Krisostomus
latviešu: Joans Hrizostoms
Bahasa Melayu: John Chrysostom
norsk nynorsk: Johannes Chrysostomos
português: João Crisóstomo
srpskohrvatski / српскохрватски: Jovan Hrizostom
Simple English: John Chrysostom
slovenčina: Ján Zlatoústy
slovenščina: Janez Zlatousti
српски / srpski: Јован Златоусти
Tiếng Việt: Gioan Kim Khẩu