Mbinu ya rediokaboni

Mbinu ya rediokaboni (pia: mbinu ya 14C; kwa Kiingereza: radiocarbon dating, carbon-14 dating) ni njia ya kisayansi ya kutambua umri wa mata ogania.

Msingi wa mbinu hii ni uwepo wa kaboni katika kila kiumbe; na kupungua kwa idadi ya isotopi za kaboni aina za 14C kwa sababu idadi za atomi nururifu inapungua kadiri ya mbunguo nyuklia. Kutokana na asilimia za kaboni nururifu ya 14C iliyobaki katika mata ogania inawezekana kukadiria umri wake.

Mbinu ya rediokaboni ni muhimu hasa kwa fani ya akiolojia. Mbinu hii inamruhusu mtaalamu kujua umri wa ubao, mifupa na mabaki mengine yanayotokana na viumbe wa kale.

Hata hivyo mbinu hii inahitaji kuwepo kwa mata ogania, yaani haiwezi kutambua umri wa vitu kama dhahabu, chuma, mwamba.

Vilevile haiwezi kuleta matokeo kwa viumbe wenye umri mkubwa kushinda miaka 60,000.

Historia ya mbinu hii

Mbinu hii ya upimaji iligunduliwa mnamo 1946 na mtaalamu Mmarekani Willard Frank Libby aliyepokea tuzo ya Nobel ya Kemia mwaka 1960. Libby aliweza kuonyesha usahihi wa mbinu yake kwa kutambua umri wa mbao za jeneza na za boti ya Misri ya Kale. Jeneza na boti zilihifadhiwa katika makaburi ya Misri ambako vitu vingi vimekaa tangu miaka elfu kadhaa bila kuoza kutokana na hewa kame ya nchi hiyo. Hali nzuri ya yaliyomo katika makaburi ya Misri imetunza pia maandiko juu ya vitu hivyo ambayo mara nyingi pia hutaja mwaka wa kifo cha mhusika wa kaburi, na hivyo kutaja umri wa kaburi. Upimaji wa Libby ulilingana na umri uliojulikana tayari, hivyo kuthibitisha uwezo wa mbinu yake.[1]

Other Languages
Bahasa Indonesia: Penanggalan radiokarbon
Nederlands: C14-datering
norsk nynorsk: Radiokarbondatering
srpskohrvatski / српскохрватски: Radiokarbonsko datiranje
Simple English: Radiocarbon dating